Isome Hapa Hotuba ya Rais Trump
Isome Hapa Hotuba ya Rais Trump

TRUMP: Jaji Mkuu Roberts, Rais Carter,
Rais Clinton, Rais Bush, Rais Obama, Wamarekani wenzangu na watu wote
duniani, asanteni sana. (MAKOFI)
Sisi, Wananchi wa Marekani, tunaungana katika juhudi za pamoja kitaifa
kujenga nchi yetu na kutunza ahadi zake kwa watu wetu wote. (MAKOFI)
Pamoja, tutaamua hatima ya Marekani na dunia kwa ajili ya watu wote (na
tutafanya hivyo) kwa miaka mingi ijayo. Tutakutana na changamoto,
tutakutana na vikwazo, lakini tutahakikisha kazi inafanyika.
Kila miaka minne, tunakusanyika hapa kubadilishana madaraka kwa njia ya
amani, na tunamshukuru sana Rais Obama na mke wa Rais Bi. Michele Obama
kwa msaada wao mkubwa muda wote tulipokuwa tunafanya mchakato huo.
Wamekuwa watu muhimu. Asanteni sana. (MAKOFI)
Pamoja na hayo, sherehe ya leo, ina maana kubwa, hatuko hapa kwa ajili
tu ya kuhamisha madaraka kutoka utawala mmoja kwenda mwingine au kutoka
chama kimoja kwenda chama kingine, lakini tuko hapa kuhamisha madaraka
kutoka Washington D.C na kuyakabidhi kwenu, watu. (MAKOFI).
Kwa muda mrefu, kikundi kidogo kwenye mji mkuu wa nchi yetu kimekuwa
kikivuna matunda ya serikali wakati watu wakibeba gharama. Washington
iliendelea kuneemeka lakini watu hawakupata mgao wa utajiri wake.
Wanasiasa walifaidika lakini kazi ziliondoka na viwanda vikafungwa.
Mfumo wa Waanzilishi (The Establishments) ulijilinda na siyo kuwalinda
wananchi wa nchi yetu. Ushindi (wa Waanzilishi) haukuwa ushindi wenu.
Mafanikio yao hayakuwahi kuwa mafanikio yenu. Na wakati walikuwa
wakisheherekea kwenye mji mkuu wa nchi yetu, familia zinazohangaika nchi
nzima hazikuwa na cha kusheherekea. (MAKOFI)
Mabadiliko yote hayo yanaanzia hapa na yanaanza sasa hivi kwa sababu
wakati huu ni wakati wenu na ni wakati unaomilikiwa na nyinyi. (MAKOFI)
TRUMP: Wakati huu unamilikiwa na kila mmoja aliyekusanyika hapa leo na
kila mmoja anayetufuatilia akiwa sehemu yoyote hapa Marekani. Hii ni
siku yenu. Hii ni sherehe yenu. Na hii, Marekani, ni nchi yenu.
(MAKOFI).
Cha msingi siyo chama gani kinaongoza serikali yetu, cha msingi ni ikiwa serikali yetu inadhibitiwa na nyinyi, watu. (MAKOFI).
Tarehe 20 Januari 2017 itakumbukwa kama siku ambayo watu (Wa Marekani) walikuwa watawala wa taifa hili tena. (MAKOFI).
Wanaume na Wanawake wa nchi yetu hawatasahaulika tena. (MAKOFI).
Kila mmoja anawasikiliza hivi sasa. Mmekuja kwa wingi mno kwa makumi na
mamilioni kuwa sehemu ya vuguvugu, mfano ambao dunia haikuwahi kuuona
kabla. (MAKOFI).
Katikati ya vuguvugu hili kuna ahadi muhimu, kwamba taifa lipo kwa ajili
ya kuwatumikia raia wake. Wamarekani wanahitaji shule bora kwa ajili ya
watoto wao, majirani salama kwa ajili ya familia zao, kazi nzuri kwa
ajili yao. Haya ni mahitaji halali na ya msingi ya watu sahihi na jamii
sahihi.
Lakini sehemu kubwa ya watu wetu, wanakumbana na halisia tofauti: akina
mama na watoto wameshikiliwa na umasikini ndani ya miji yetu; viwanda
vilivyochakaa vimetapakaa kama makaburi kila kona ya nchi yetu; elimu
yetu inatolewa kwa wenye pesa, jambo linaloacha wanafunzi wetu wadogo na
wazuri wakinyimwa maarifa; na uhalifu na makundi ya kihalifu na madawa
ya kulevya ambavyo vimeshachukua maisha ya watu wengi na kuiondolea nchi
yetu nguvu kazi muhimu. Mabalaa hayo kwa Wamarekani yanasimamishwa
mahali hapa na yanasimama sasa hivi. (MAKOFI)
Sisi ni taifa moja na maumivu yao ni maumivu yetu. Ndoto zao ni ndoto
zetu. Na mafanikio yao yatakuwa mafanikio yetu. Tunashirikishana moyo
mmoja, nyumba moja na matarajio ya aina moja. Kiapo cha Urais
nilichokula leo ni kiapo cha utii kwa Wamarekani wote. (MAKOFI).
Kwa miongo mingi, tumekuwa tukitajirisha viwanda vya nje ya Marekani kwa
gharama za viwanda vya Marekani; tumekuwa tukitoa ruzuku na kuyapa
majeshi ya nchi nyingine, wakati tukiruhusu hali mbaya na ya kusikitisha
kwa majeshi yetu. Tumekuwa tukilinda mipaka ya nchi nyingine na
tukikataa kulinda mipaka yetu wenyewe. (MAKOFI).
Tumekuwa tukitumia trilioni na trilioni za dola za Marekani nje ya nchi
yetu wakati miundombinu ya Marekani ikiwa imeanguka, kuharibika na
kuoza. Tumekuwa tukizifanya nchi nyingine kuwa tajiri, wakati utajiri,
uimara na kujiamini kwa nchi yetu kukipungua kwa kila namna.
Kimoja baada ya kingine, viwanda vikafungwa na vikaiacha ardhi yetu,
bila hata kufikiria kuhusu mamilioni na mamilioni ya Wamarekani ambao
walikuwa wanapotezewa kazi. Utajiri wa watu wa kati umeondolewa kutoka
kwenye familia zao na kisha ukagawanywa katika nchi zote duniani. Lakini
hayo yamepita. Na sasa, tunaangalia mbele tu. (MAKOFI).
TRUMP: Tumekusanyika hapa leo kutoa AMRI MPYA itakayosikika katika kila
mji, katika kila mji mkuu wa nchi za Dunia yote, na katika kila sehemu
yenye madaraka. Kuanzia leo kwenda mbele, dira mpya ndiyo itaongoza
taifa letu. Kuanzia leo kwenda mbele, itakuwa ni Marekani kwanza,
Marekani kwanza. (MAKOFI).
Kila maamuzi kuhusu biashara, kuhusu kodi, kuhusu uhamiaji, kuhusu mambo
ya nje yatafanywa kuwanufaisha wafanyakazi wa Marekani na familia za
Marekani. Lazima tulinde mipaka yetu dhidi ya mipango ya nchi nyingine
kutengeneza bidhaa zetu, kuiba makampuni yetu na kuharibu kazi zetu.
(MAKOFI).
Kujilinda kutapelekea tupate uimara na mafanikio makubwa. Nitawapigania
kwa kila pumzi iliyomo kwenye mwili wangu. Na kamwe sitaawangusha.
(MAKOFI).
Marekani itaanza kushinda tena, kushinda kuliko ilivyowahi kutokea. (MAKOFI).
Tutarudisha kazi zetu. Tutarudisha mipaka yetu. Tutarudisha utajiri wetu. Tutarudisha ndoto zetu. (MAKOFI).
Tutajenga njia mpya, na njia kuu na madaraja na viwanja vya ndege na
mitaro na reli kila mahali katika nchi yetu kuu. Tutawatoa watu wetu
kwenye matatizo na kuwarudisha wafanye kazi, kuijenga upya nchi yetu kwa
mikono ya Wamarekani na Wafanyakazi wa Marekani. (MAKOFI).
Tutafuata kanuni mbili za kawaida; nunua Mmarekani na ajiri Mmarekani
(Nunua bidhaa ya Marekani na toa ajira kwa Raia wa Marekani). (MAKOFI).
Tutatafuta marafiki na kuonesha nia njema kwa mataifa ya dunia, lakini
tutafanya hivyo kwa kuelewa kwamba ni haki ya kila taifa kuweka mbele
maslahi yake.
Hatutatafuta kuanzisha aina yetu ya maisha kwa taifa lolote, lakini
badala yake kufanya maisha yetu yangare na kuwa mfano. Tutangara ili
kila taifa lifuate mfano wetu. (MAKOFI).
Tutarejesha marafiki wa zamani na kukaribisha wapya na kuunganisha dunia
iliyostaarabika dhidi ya Ugaidi wa Uislamu wa siasa kali, ambao
tutauondoa katika uso wa dunia. (MAKOFI).
Katika kitovu cha siasa zetu kutakuwa na utii mkubwa kwa Marekani, na
kupitia heshima kwa nchi yetu tutavumbua heshima kwa kila mmoja.
Unapofungua moyo wako kwa ajili ya uzalendo, hakutakuwa na nafasi ya
kuhujumiwa. (MAKOFI).
Biblia inatueleza namna ilivyo jambo jema pale watu wa Mungu wanapoishi
pamoja katika muunganiko/muungano. Lazima tuseme yaliyomo katika fikra
zetu kwa uwazi, tujadiliane mambo ambayo hatukubaliani kwa uaminifu,
lakini muda wote tukilinda umoja wetu. Wakati Marekani inapoungana,
hakuna awezaye kuisimamisha. (MAKOFI).
Hakupaswi kuwa na woga. Tunalindwa na siku zote tutalindwa. Tutalindwa
na wanaume na wanawake wasio na mfano ambao wako kwenye majeshi yetu na
vyombo vya dola. Na muhimu kuliko yote, tutalindwa na Mungu. (MAKOFI).
TRUMP: Mwisho, lazima tufikiri mbali na kuota ndoto kubwa zaidi.
Marekani, tunafahamu kwamba taifa linaishi ikiwa tu linapambana kupata
matokeo bora. Hatutaendelea kukubali wanasiasa ambao wanaongea bila
vitendo, muda wote wanalalamika, lakini hawajawahi kufanya chochote ili
kubadilisha kile wanachokilalamikia. (MAKOFI)
Muda wa mazungumzo hewa umekwisha. Sasa imefika saa ya vitendo. (MAKOFI).
Usiruhusu mtu yeyote akwambie kwamba haiwezi kufanyika. Hakuna
changamoto inayoweza kuendana na jitihada na ari ya Marekani.
Hatutashindwa. Nchi yetu itavuka na kushamiri tena.
Tunasimama wakati wa kuzaliwa kwa milennia mpya, tukiwa tayari kufungua
majaribu ya anga, kuifanya dunia kuwa huru dhidi ya majanga ya magonjwa,
na kujenga nishati, viwanda na teknolojia kwa ajili ya kesho. Tunu mpya
za taifa zitakuwa ndani yetu, zitainua maono yetu na kuponya
migawanyiko yetu.
Ni muda wa kukumbuka busara za zamani ambazo wanajeshi wetu hawawezi
kusahau, kwamba hata kama sisi ni weusi au kijivu au weupe, sote
tunavuja damu moja nyekundu ya wazalendo. (MAKOFI).
Sote tunafurahia uhuru wa kipekee na sote tunaipiga saluti, bendera moja kuu ya Marekani. (MAKOFI).
Na ikiwa mtoto amezaliwa katika eneo la Mjini la Detroit au maeneo yenye
upepo mwingi huko Nebraska, wote wanaangalia anga moja ya usiku, wote
wana ndoto moja, na wote wamepewa pumzi ya maisha na Muumbaji mmoja.
(MAKOFI).
Kwa hiyo, kwa Wamarekani wote katika kila mji karibu na mbali, mdogo na
mkubwa, mlima kwa mlima, bahari kwa bahari, sikilizeni maneno haya.
Hamtadharauliwa tena. (MAKOFI).
Sauti zenu, matumaini yenu na ndoto zenu, zitaeleza ukuu wa Marekani
yetu. Na ujasiri wenu na uzuri wenu na mapenzi yenu vitatuongoza siku
zote katika njia tunayopita. (MAKOFI).
Pamoja, tutaifanya Marekani kuwa imara tena. Tutaifanya Marekani kuwa
tajiri tena. Tutaifanya Amerika kujivuna tena. Tutaifanya Marekani kuwa
salama tena. Na ndiyo, pamoja tutaifanya Marekani kuwa Kuu tena.
(MAKOFI).
Asanteni sana. Mungu awabariki. Na Mungu aibariki Marekani. (MAKOFI).
Na. Mtatiro J (Imefasiriwa na JSM).
Baruapepe: juliusmtatiro@yahoo.com, Whatsup: +255 787 536759.
Comments